missing

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 13/09/2020Mimba za umri mdogo zinauwa- TAMWA, ZNZ

Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kinaiomba jamii kusaidia kutoa elimu dhidi ya athari ya mimba na ndoa za umri mdogo ili kuwanusuru watoto na majanga ambayo yanawaathiri kimwili na kisaikolojia na wengine hupoteza maisha.

Tatizo hilo litaweza kuondoka endapo nguvu za pamoja zitaungana, wakiwemo viongozi wa dini, wanasiasa, wanaharakati wa masuala ya wanawake, kupanga mikakati mahsusi ya kuelimisha jamii athari zinazojitokeza wakati wa kjifungua katika umri mdogo.

TAMWA, ZNZ hivi karibuni imepokea taarifa za kusikitisha za mtoto aliyechini ya umri wa miaka 15 aliyebakwa na kupata ujauzito/mimba na hatimae kupoteza maisha wakati wa kujifungua.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mzazi wa marehemu zinasema tukio hilo limetokea wilaya ya Wete, Mkoa wa kaskazini Pemba na kwamba marehemu alifariki tarehe 25 /06/2020 wakati akijifungua.

TAMWA, ZNZ kimefanya uchunguzi kuhusiana na athari za mimba za mapema na kugundua kuna madhara mengi ambayo yanajitokeza katika mimba za mapema ikiwemo kuathirika kimwili na kisaikolojia pamoja na kupoteza maisha, hivyo jitihada za pamoja zinahitajika katika kupambana na janga hili linalowaathiri watoto ambao ndio taifa la kesho.

Kwa mujibu wa wataalam wa afya, Daktari Kamilia Ali Omar wa kitengo cha wazazi katika Hospitali ya Mnazi mmoja Zanzibar amesema mimba za umri mdogo zinaweza kusababisha ugonjwa wa Fistula, saratani ya shingo ya kizazi na magonjwa mengine hujitokeza kutokana na baadhi ya maungo katika mwili hayajapea.

“Kujifungua chini ya miaka 18 ni kuhatarisha maisha ya mama na  mtoto kwa sababu nyonga ya mtoto aliyechini ya miaka 18 haijapea/komaa na kuweza kusukuma mtoto hivyo hupelekea mzazi kuwa katika hali hatarishi ya kupata ugonjwa wa fistula, au mzazi hupoteza maisha au baadhi ya maradhi huenda yakajitokeza kwa baadae” amesema Dkt Kamailia.

Dkt Kamilia amesema wataalam wa afya wanashauri umri wa kujifungua angalau msichana afikie/atimize miaka 20 hadi 22.

Hivyo ameshauri endapo tatizo la mimba china ya umri litajitokeza kwa mtoto ni vyema kuwahishwa kliniki mapema ili wataalum wa afya wamuweke chini ya uangalizi kwa ajili ya kunusuru maisha ya mama na  mtoto.

Kwa upande wa mwanasaikolojia kutoka Zanzibar Skuli of Health Bi Asya Saleh Abdullatif amesema mimba za mapema zinapelekea msongamano wa mawazo ambayo yanaweza kusababisha mhanga wa mimba za mapema kuzimia au kupata ugonjwa wa akili.

Pia Bi Asya amesema mimba za umri mdogo hupelekea hasira za mara kwa mara ambapo mhanga anaweza kufanya kitendo kibaya dhidi yake au kwa mtu mwengine ambacho kitaweza kuleta madhara.

TAMWAZNZ imebaini mimba za mapema kujitokeza katika hali nne, kwa mtoto kubakwa, kuozeshwa kwa nguvu, kuozeshwa mapema au kwa kuhadaiwa.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imeainisha jumla ya mimba 88 za umri mdogo na ndoa za umri mdogo 50 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Kwa hiyo, hizo ni takwimu kwa upande wa elimu tu ambazo mara nyingi hupatikana baada ya watoto kukatisha masomo kwa sababu za ujauzito au kuolewa.

Ni yumkini kabisa kuwa kuna wasichana wengine kwenye jamii ambao waliacha kwenda shule zamani ama hawakwenda shule tokea awali na taarifa zao kutokurikodiwa.

 Ni vizuri sana jamii kufahamu tatizo hili la mimba za utotoni ili kunusuru maisha ya wasichana hao na pia kwa Serikali kuchukua hatua kali kwa watu ambao wanabaka watoto hao ama kuwaozesha kwa nguvu ili kumaliza tatizo hilo.

Dkt Mzuri Issa

Mkurugenzi,

TAMWA Zanzibar

 

Contact us

TAMWA ZANZIBAR
P.O.Box 741,
TUNGUU ZANZIBAR
Phone: +255772378378
Email: info@tamwaznz.org

Get Our Latest News

To get our news updats please insert your email and subscribe


© Copyright 2020 Tanzania Media Women's Association. All Rights Reserved